Have a question?
Message sent Close

Utangulizi

Tarehe 7 Julai tunasherehekea siku ya kimataifa ya kiswahili, hii ni siku muhimu ambayo inatukumbusha kukienzi, kukikuza na kukieneza kiswahili. Awali uamuzi wa kutenga siku hii ulichukuliwa na shirika la umoja wa mataifa la UNESCO mwezi novemba 2021 na tarehe mosi ya mwezi  wa saba 2024, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha siku ya tarehe 7 Julai kuwa siku ya kiswahili duniani. Uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO na baadaye Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unakifanya kiswahili kuwa lugha pekee ya kiasili kutoka Bara la Afrika ambayo imepata hadhi hii ya Kimataifa.

Watu wengi wamejiuliza kwanini kiswahili? Napenda ifahamike bara la Afrika lina makabila yanayozungumza lugha tofauti tofauti zaidi ya 2000. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania peke yake ina makabila yanayozungumza lugha zaidi ya 120. Nyingi ya lugha hizi ziko kimaeneo, na mifano ya lugha hizo ni pamoja na Kiyoruba, kinazungumzwa katika nchi za Nigeria, Benin, na Togo. Lugha ya Kizulu inazungumzwa zaidi nchini Afrika ya Kusini. Mfano mwingine ni lugha ya Kihausa kinachozungumzwa zaidi Afrika Magharibi katika nchi za Nigeria, Ghana na Niger na ni lugha ya pili katika nchi za Benin, Cameroon, Togo, Ivory Coast and Sudan. Kiswahili hata hivyo, mpaka sasa ndio kinacho ongoza kwa kuwa na wazungumzaji wengi, zaidi milioni 200 na kinazungumzwa kama lugha kuu na lugha ya pili kwenye zaidi ya nchi 15 za Afrika na kina wazungumzaji katika nchi nyingi zaidi nje ya Bara la Afrika.

Bado nitajiuliza kwanini kiswahili? Napenda ifahamike tofauti na lugha nyingine za Afrika, kiswahili kina utajiri wa mchanganyiko wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani na walioleta lugha mbalimbali, tamaduni, desturi, imani na taratibu zao.

Awali kabisa, kiswahili kilienea kutoka pwani za Tanganyika na Kenya katika karne ya 18 na wahusika wakuu walikuwa wafanyabiashara waliosafiri kwa misafara kutoka pwani mpaka ndani ya bara la Afrika ikiwemo Congo. Zilikuweko njia kadhaa za misafara ya wafanyabiashara kutoka pwani ya Afrika Mashariki kwenda ndani kabisa ya bara la Afrika na katika kila miji ya njiani kiswahili kilitumika kama lugha ya mawasiliano na biashara.

Huu utajiri wa mchanganyiko wa watu, lugha zao, tamaduni zao, desturi zao, imani zao unaifanya lugha ya kiswahili kuwa na sifa ya lugha ambayo inavuka zaidi ya kabila moja au zaidi ya jamii moja na hivyo kuifanya kuwa lugha kubwa kwa matumizi, kwa kutandaa na kwa kutumika kama lugha ya kwanza au ya pili. Ukubwa huu wa lugha ya kiswahili ni tofauti na lugha nyingine kongwe ambazo zimeshikamana na kabila au jamii ya watu wa eneo fulani na ambazo zinaweza kuwawezesha watu kusimama pamoja na kuwa na nguvu na maslahi binafsi hasa ya kisiasa na kiuchumi ya kabila au jamii husika dhidi ya jamii na makabila mengine. Kiswahili huwa hakina sifa hiyo, hakina kabila wala hakina milki ya kundi fulani.

Wanazuoni wanafafanua kwamba kiswahili ambayo ni lugha inayovuka kabila au jamii za watu imepitia hatua kadhaa katika ukuaji wake. Hatua ya kwanza ni mchango wa watu wa mashariki ya kati (waarabu), dini na utamaduni wa kiislamu, maneno na misamiati mingi ya kiswahili imeazimwa kutoka katika lugha ya kiarabu, dini na utamaduni wa kiislamu. Hatua ya pili ni mchango wa wa watu wa magharibi na wakristo na kipindi hiki lengo la kueneza ukristo umetumika kukuza matumizi na kukieneza kiswahili, hili linadhibitishwa na uwepo wa maneno mengi ambayo yameazimwa moja kwa moja kutoka katika ukristo. Hatua ya tatu ni matumizi yasiyo ya kidini ya lugha ya kiswahili hususani matumizi ya lugha ya mawasiliano ya kiserikali ikiwemo, Utawala, mahakama na vyombo vya uwakilishi. Hatua ya nne ni matumizi makubwa ya lugha ya kiswahili barani Afrika na duniani kwa ujumla na msukumo wa matumizi ya kiswahili katika sayansi, ubunifu na uvumbuzi.

Tulikotoka: Harakati za Ukombozi wa Afrika

Kiswahili tangu mwanzo kimejijengea hadhi na heshima ya kuwa lugha ya kukataa ukoloni na ukoloni mambo leo, kuanzia vita vya kuwazuia wakoloni wa kijerumani, kiswahili kilitumika kama lugha ya kuhamashisha umma kukataa uvamizi wa wajerumani, mfano mzuri ni vita vya maji-maji katika eneo kubwa la Tanganyika. Wapiganaji waliaminishwa kwamba baada ya mazingatio fulani fulani basi risasi za majeshi ya ujerumani zitakapopigwa kwa majeshi ya wenyeji zingegeuka maji. Najua sharti moja ilikuwa wapiganaji wasikutane na wenza wao wakati wa vita, vita ile wajerumani walishinda lakini vita ya majimaji ilikuwa mojawapo ya hatua za awali kuukataa uvamizi wa wakoloni katika namna ya harakati na vuguvugu lenye uratibu rasmi wakitumia kiswahili.

Ukifuatilia kwa karibu hata wakoloni kabla hawajaja rasmi barani Afrika, tayari mawakala wao walifika barani Afrika wakizungumza kiswahili ili kuwa na urahisi wa kuzungumza na wenyeji. Maandiko kadhaa yanaonesha msingi huo wa kutambua ukubwa wa kiswahili ndio uliopelekea kwa mfano ukoloni wa kijerumani Afrika Mashariki kuanza kutumia kiswahili kama lugha yao ya Utawala. Ushahidi unaonesha pia kwamba kiswahili kilianza kufundishwa kitaaluma kama lugha ya kimkakati ya kuendeleza maslahi ya wajerumani Afrika tangu miaka ya 1875 ikianza kama Seminar of Oriental Studies na baadaye kigoda cha kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kaiser Wilhelm, nchini Ujerumani.

Harakati za ukombozi na hasa vuguvugu la vyama vya wafanyakazi katika eneo lote la Afrika Mashariki, lugha ya hamasa ilikuwa kiswahili. Ilikuwa wakati huu pia na baada ya vita ya kwanza ya dunia watu wa Afrika Mashariki walianza kuona madhira ya ukoloni, ubaguzi, kunyonywa na kuonewa na kukaanza kujengeka ari ya Utaifa (nationalism) ambao ulikuwa unavuka utambulisho wa makabila ambayo yalikuwepo tangiepo na utambulisho mpya na namna rasmi ikawa lugha ya kiswahili. Radio za kitaifa wakati ule katika Afrika Mashariki zilisukuma ukuaji wa kiswahili lakini katika katika ngazi ya utawala vyombo vya dola ikiwemo polisi, mgambo na Jeshi ili kuajiriwa huko kiswahili kilikuwa kigezo kimojawapo na lugha ya mafunzo na kazi.

Chama cha TANU mwaka 1954 kilitangaza kiswahili kuwa lugha itakayotumika kutuleta pamoja katika harakati ya kupigania uhuru wa Tanganyika, uhalisia wa matumizi ya lugha ya kiswahili ulijionesha katika harakati za ukombozi wa eneo lote la Afrika Mashariki. Mwaka 1967 Tanzania ilitoa Azimio la Arusha ambalo lililenga kujenga Taifa la kijamaa na msingi muhimu ukawekwa kwamba lugha ya kiswahili ndio lugha rasmi ya kiserikali na lugha ya kufundishia katika shule za awali na msingi. Kule Kenya baada ya uhuru kiswahili kilikuwa lugha ya Taifa na kiingereza kikiwa lugha ya kiserikali na mwaka 1974 Serikali ya Kenya ilianza kutumia kiswahili katika Bunge la Kenya. 

Kwa upande wa Uganda, mpaka mwaka 1972 Kiswahili kilikuwa zaidi lugha ya kibishara kuliko ya kisiasa. Baadaye kiswahili kilitumika sana na jeshi wakati wote wa utawala wa kijeshi. Mwaka 1986 baada ya kuingia madarakani kwa Mhe. Yoweri Kaguta Museveni kiswahili kilipata msukuma mpya na hata chama tawala kilianza kutumia kiswahili kama lugha rasmi na wezeshi ya kuwafikia watu.

Mwalimu Nyerere aliamini uhuru wa Tanganyika na baadaye Tanzania haukuwa kitu kama nchi nyingine za Afrika zilikuwa bado chini ya minyororo ya wakoloni. Tanzania ilipewa na Organaizesheni ya Umoja wa Afrika (OAU) jukumu la kuongoza harakati za ukombozi wa Afrika na kwa umahususi nchi za kusini mwa Afrika. Tanzania imehusika moja kwa moja kwenye harakati za ukombozi katika nchi za Msumbiji, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Angola, Namibia, Botswana, Comoro na Seychelles.

Ushiriki wa Tanzania ulikuwa kwa maana ya kutoa msaada wa kiufundi kwa wapiganaji na harakati za ukombozi katika nchi hizo, kutoa wapiganaji kwenda mstari wa mbele sambamba na wapiganaji wa nchi mwenyeji dhidi ya wakoloni, kutoa misaada ya kifedha na kuanzisha makambi ya mafunzo kwa wapigania uhuru wa nchi tajwa kuja kushiriki mafunzo ya kijeshi.

Wakati wote wa harakati za ukombozi, lugha ya kiswahili ilitumika kama lugha fiche na ya kimkakati katika mawasiliano na uratibu wa mapambano katika makao makuu ya Kamati ya Ukombozi Dar Es Salaam na katika uwanja wa mapigano katika nchi za kusini mwa Afrika. Wapigania uhuru wote walifundishwa mafunzo ya umahiri na kijeshi kwa kutumia kiswahili. Kiswahili kilikuwa lugha fiche na ya kimkakati katika mawasiliano ukizingatia majeshi ya wakoloni wa kireno na makaburu walikuwa hawajui lugha hii na hii ilipelekea mafanikio makubwa katika uwanja wa mapambano.

Mwaka 1965 wapiganaji takribani 100 kutoka nchini Cuba walielekea katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutekeleza jukumu maalum wakiwezeshwa kupitia nchini Tanzania na wakiongozwa na Makamanda Ernesto Guevara de la Serna, Victor Dreke na Jose Maria Martinez Tamayo. Wapiganaji hawa pia kama sehemu ya mikakati ya kufanikiwa kwa jukumu hilo maalumu walilazimika kujifunza kiswahili ikiwemo kupewa majina fiche ya kiswahili. Kamanda Kiongozi Che Guevara aliitwa “Kamanda namba tatu”, Kamanda Tamayo aliitwa “Kamanda namba Mbili” na kamanda Dreke aliitwa “Kamanda namba Moja”.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa alitembelea nchi ya Cuba mwaka 1974 na baadaye Amiri Jeshi Mkuu wa Mapinduzi ya Cuba Fidel Castro Ruz na Rais wa Jamhuri ya Cuba alitembelea nchi ya Tanzania. Ziara za viongozi hawa zilipelekea kuanza kwa jitihada za kufundisha kiswahili nchini Cuba na Tanzania kupokea wanafunzi vijana kutoka Cuba kuja kujifunza kiswahili nchini Tanzania. Zoezi hili la ufundishaji wa kiswahili lilitekelezwa kwa takribani miaka mitano na likasimama. 

Kiswahili ni utamaduni, ni mtindo wa maisha, na waswahili wameenea kote ulimwenguni na wanajivuna kuwa waswahili. Hata kule nchini Marekani, jamii ya wamarekani weusi ambao kihistoria walitokea Afrika wamekuwa mstari wa mbele kutumia kiswahili kuenzi asili yao. Mfano mzuri ni vuguvugu na maadhimisho ya “Kwanzaa” nchini Marekani, neno ambalo linamaanisha “mwanzo” na huhusisha sherehe za mavuno ya kwanza katika jamii za zamani barani Afrika. Toka miaka ya 1960, Waadhimishaji wa Kwanzaa wanahusianisha maisha ya waafrika na ujamaa na kiswahili kikiwa ni lugha na utamaduni wao. Kwanzaa inatambua na kuenzi misingi kadhaa ikiwemo umoja, kujichagulia, ujima, ujamaa, nia, kuumba na imani.

Pasina shaka, kiswahili kimekuwa lugha ya kimapinduzi, lugha ya kiumajumui, kiswahili kimekuwa lugha ya kuwaunganisha wanyonge ili kudai na kutetea haki zao dhidi ya wanyonyaji.

Tuliko: Kiswahili lugha, utamaduni na bidhaa

Ni furaha kubwa kwamba nchi za Tanzania na Cuba zimeanzisha tena rasmi mafunzo ya kiswahili nchini Cuba. Mafunzo ya kiswahili yanatolewa katika Chuo Kikuu cha Havana na Katika Nyumba ya Utamaduni wa Afrika. Lengo la muda mfupi ni kuendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi ya kiswahili katika maeneo haya mawili na lengo la kati likiwa ni kuwezesha wanataaluma 10 kwenda kujifunza kiswahili nchini Tanzania katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na halkadharika, wanataaluma 10 kutoka Tanzania kuja kujifunza lugha ya kihispaniola katika Chuo Kikuu cha Havana. Lengo letu kuu ni kushirikiana kwa Serikali zetu mbili za Tanzania na Cuba na taasisi zake kukifikisha kiswahili katika ukanda wa Karibe, America ya Kati na Amerika ya Kusini.

Leo hii Kiswahili ni kati ya lugha 10 maarufu duniani, ndio lugha ya kiasili kutoka bara la Afrika ambayo imekua kwa haraka na kupata utambulisho wa Kimataifa. Kuna mamia ya vyuo vikuu duniani vinavyofundisha kiswahili ikiwemo zaidi ya 100 nchini Marekani. Katika Umoja wa Mataifa, kuna lugha 6 zinazotumika na kila lugha ina siku yake ya kimataifa. Kiswahili na Kireno ndio lugha pekee ambazo sio lugha rasmi za Umoja wa Mataifa lakini umoja wa Mataifa umezipa hadhi ya kuwa na siku za Kimataifa kwa kutamkwa na Umoja wa Mataifa. Kimsingi hii ni heshima kubwa ambayo lugha ya kiswahili imestahili na imekuja kwa kuchelewa, hatua inayofuata ni Kiswahili

kutamkwa kuwa lugha rasmi ya saba katika Umoja wa Mataifa.

Kiswahili sasa ni lugha rasmi na ya kazi ya taasisi za kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika (AU), Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Mizizi ya kiswahili sasa imeenea katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Sudani Kusini, Somalia, Msumbiji, Malawi, Zambia, Comoros, Seychelles, Oman, Yemen na Mashariki ya Kati.

Tayari nchi kadhaa za kusini mwa Afrika zimeanza kutambulisha lugha ya kiswahili katika mifumo yao ya elimu, nchi hizo ni pamoja na Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Ethiopia, Namibia na Malawi. 

Kama sehemu ya jitihada za Serikali mbili za Tanzania na Cuba kukuza kiswahili, imependekezwa kwamba kiswahili kifundishwe na wacuba hapa Cuba na kihispaniola kifundishwe nchini Tanzania na watanzania wenyewe. Kamusi ya Kihispaniola na kiswahili inaendelea kuandikwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na Chuo Kikuu cha Havana. Aidha kijitabu cha misemo kinakamilishwa ambacho kitakuwa na lugha za Kiswahili, Kihispaniola na Kiingereza ili kurahisisha kujifunza na matumizi ya kawaida ya lugha ya kiswahili.

Ukizingatia asili ya watu wengi katika ukanda huu, utagundua asili yao ni Bara la Afrika, biashara ya utumwa ilileta watu ambao walifika hapa na tamaduni zao. Ukichunguza kwa karibu utagundua uhusiano wa karibu sana kati ya tamaduni za watu wenye asili ya Afrika katika ukanda huu na tamaduni zilizoko barani Afrika. Mifano michache ni uwepo wa imani ya kiyoruba, ambayo iko pia Afrika na kama nilivyoeleza awali kwa maana ya lugha ya kiyoruba. Ukitizama ngoma ya konga hapa Cuba inafanana sana na ngoma ya mdundiko kwa tabia zake, ngoma ya konga kama kule Santiago De Cuba ikipigwa mtaani basi ujue watoto wadogo watakwenda kufuata konga, kama mama alikuwa anapika anaweza akaacha chakula kwenye moto jikoni akafuata konga na mara kadhaa watoto huweza kupotea wazazi wasipokuwa makini, kwa Tanzania huo ndio mdundiko.

Nguvu ya muziki wenye asili ya Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umekuwa maarufu sana katika nchi ya Colombia katika mji wa Cartagena, wanasikiliza nyimbo za kiswahili, wanacheza “bolingo”, wanakatika kama tunavyokatika sisi tunapocheza muziki wa bolingo na muziki wa kutoka congo. Kijiji cha San Basilio Del Palenque ndio mji wa kwanza kwa watumwa kujiweka huru katika eneo lote la Latini Amerika, na wameendelea kuenzi tamaduni na desturi za kiafrika. Kazi moja imebaki ni kwa serikali za Afrika, Karibe, Amerika ya Kati na Amerika ya Kusini kuendelea pale ambapo juhudi za watu wa pande zote mbili wamefika katika kuenzi utamaduni unaoonesha uhusiano wa karibu kati ya bara la Afrika na ukanda huu. 

Kipindi hiki kiswahili ni bidhaa pia, machapisho, maandiko mbalimbali, vitabu vya kiada na ziada, vitabu vya hadithi, vitabu vya riwaya, kamusi mbalimbali, yote haya yanahitajika kuwafikia watumiaji wapya wa kiswahili katika ukanda huu. Hii fursa kubwa kwa wachapishaji wa vitabu, wahariri, waandishi wa vitabu vya aina zote na hata wachambuzi wa vitabu. 

Tunakoelekea: Utangamano wa Kidunia 

Iko fursa kubwa sana kwa nchi zinazoendelea na za kusini kushirikiana kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Katika miaka ya sitini, wanazuoni kadhaa walifika katika bara la Afrika na kufanya kazi huko katika Serikali na vyuo Vikuu nitaje wawili kwa mfano nao ni Walter Rodney na Prof. Clive Thomas kutoka Guyana, hawa wanafahamika sana Tanzania na Afrika.

Ifahamike katika ulimwengu wa leo, bara la Afrika ndio bara lenye kila aina ya rasilimali zinazohitajika kote duniani. Asilimia 60 ya ardhi ya kilimo na yenye rutuba iko barani Afrika. Dhahabu, Almasi, Tanzanite, Bauxite, Graphite, Uranium, Coal, Gesi asilia, Gesi ya Helium nikitaja kwa uchache. Hivi karibuni kumegunduliwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika, madini yasiyopatikana kirahisi na ya kimkakati na yanayosaidia dunia kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyosafi kwenda nishati safi na isiyo haribu mazingira. Tunatamani utajiri huo wa Afrika tuwashirikishe ndugu zetu mlioondoka Afrika zamani na kuja kuishi katika ukanda huu.

Bara la Afrika linaendelea na mchakato wake wa kuifanya Afrika kuwa moja, kama alivyosema mwanazuoni mmoja kwamba Umajumui wa Afrika ndio mama, utangamano wa Afrika ndio mtoto na chakula cha mtoto ni lugha ya kiswahili. Uhusiano imara wa nchi za Afrika, Karibe, Amerika ya Kati na Amerika ya Kusini katika maeneo ya Kiuchumi, Kisiasa, Kidiplomasia, Kiutamaduni na Kiteknolojia unapaswa kushajihishwa na lugha ya kiswahili. 

Ikumbukwe, lugha ya kiswahili itakuwa inaletwa rasmi katika ukanda huu kupitia Kongamano la Kimataifa za Kiswahili litakalofanyika Jijini Havana likiwa limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba, Mwezi Novemba 2024, shime karibuni nyote kushiriki tukikaribishe kiswahili katika ukanda huu.

Asanteni sana na Mungu awabariki nyote. ¡Hasta la Victoria Siempre!

Leave a Reply